*****
MLIO wa simu yake ndiyo
uliozindua kutoka katika ndoto yake ambayo hakuimalizia vizuri. Ndoto
iliyoamsha tabasamu zuri kama aamkavyo kila siku akiwa na furaha. Furaha ya
kupata kile akitakacho. Maisha aliyatamani na kuweza kuwa nayo.
Hakuwa na jinsi zaidi
ya kutii amri ya simu yake. Alijiwekea alamu tayari kwa kumwamsha kila siku.
Kaupepo kalichopenya dirishani pia hakikumpa nafasi ya kuendelea kujigubika na
shuka.
Alizitumia kama dakika
tano kujiweka sawa kabla ya kutoka kitandani. Usingizi haukumweka tena
kitandani. Alitabasamu tena kuushukuru upepo ulioumaliza usingizi wake na
kumfanya mpya tayari kwa kuianza siku
hiyo. Alijivuta hadi kushika simu yake iliyokuwa katika kijimeza kidogo pembeni
ya kitanda na kuiangalia. Hakukuta chochote zaidi ya nambari zilizoonyesha muda
wa kuamka baada ya ile alamu kuisha.
Saa kumi na moja na
nusu asubuhi ni muda ambao siku zote alijikuta yuko macho. Wakati mwingine
aliiwahi alamu ya simu yake kabla haikulia kumwamsha. Hapo alijua labda ililia
na hakuisikia na hivyo amechelewa. Alifurahi mara nyingi alipoiwahi. Alijua
kulala sana ni dalili za uvivu na hivyo hakuupa nafasi uvivu umtawale.
Wakati mwingine
hakuipenda kwani ingemaliza hamu yake ya kulala wakati bado ana usingizi, hivyo
alijua siku za kuiweka na siku za kuitoa. Ni endapo angechelewa kulala sana.
Asingeiweka na siku hiyo angeamka muda wowote na kwenda kazini.
Kama kawaida yake. Kioo
kilikuwa ni kitu cha pili baada ya kuiwasha taa yake iliyokuwa karibu na kitanda.
Taa inayowekwa mezani kwa ajili ya dharura. Mwanga hafifu uliomwangazia
ulimtosha kujiangalia usoni peke yake. Alitaka kila siku aone mabadiliko
yaliyotokea wakati akiwa amelala. Kama angeona utofauti, hakusita kwenda kwa
mtaalamu ili amsaidie. Lakini leo hakuona lolote. Alijiona vilevile kama
alivyolala jana yake saa tano na nusu usiku.
Kati ya mambo ambayo
Jane aliyahusudu sana ni jinsi alivyo. Alijua ni hulka ya wanawake kujipenda
lakini yeye aliona amewazidi kwa kujipenda alivyo. Kitu gani hakuwa nacho hadi
asijihusudu mwenyewe pindi ajiangaliapo kwenye kioo chake mwenyewe...
Aliamka sasa na
kukifuata kioo kikubwa alichokuwa amekiegemeza ukutani. Inawezekana kwa kuamka
mapema kila siku ni ile autumie muda huo kucheza na kioo. Vyumba vyake viwili
na maliwato iliyokuwa ndani ilimfanya ajisikie huru kama aishiye katika hekalu.
Yote aliyafanya ndani. Alifurahia maisha yake. Alifanya alichokitaka.
Kioo chake hakukitumia
vibaya. Sasa ilikuwa zamu ya umbo lake. Alikifuata kioo na kukisimamisha
vizuri. Alijiona wote. Alitoa shuka
ambalo alikuwa amejifunika. Alilirusha hadi kitandani kama vile alisahau bahati
mbaya akashuka nalo. Alisahau kwamba lilitakiwa limsitiri. Habari hiyo
hakuitaka. Alisimama wima. Tabasamu lilianza kuchanua taratibu. Kila ajiangaliapo
husahau kama alifanya hivyo jana yake.
Alijitazama na
kuliangaza umbo lake lililoimarika vizuri. Alijitamani. Alishika kiuno chake
kwa staili ifanywayo na walimbwende wawapo katika mashindano. Kisha akatembea
hatua mbili mbele. Alicheka. Alijikubali. Alitamani apige kelele kumshukuru
aliyemleta duniani.
Alirudi tena hatua
mbili nyuma. Sasa aligeuka kuangalia umbile lake kwa nyuma. Aliguna akimaanisha
Muumba hakumkosea. Taratibu akawa anaelekea bafuni akiwa hajaridhika.
Alilifuata bafu huku
macho yake yakiwa nyuma kumalizia kujitazama tena na tena kama hatatoka tena
alikokwenda. Huko bafuni yakawa yale yale. Kila kiungo kikisafishwa kwa nafasi
yake. Mikono yake laini ilipita kila sehemu kuhakikisha inapata sabuni
iliyokuwa inanukia pamoja na maji.
Dakika kumi zilimtosha
kujimwagia maji, si mkaaji sana wa bafuni. Alitoka. Alirudi tena kiooni. Sasa
ilikuwa ni kujikausha kwa taulo lake jeupe na safi. Alifanya hivyo akilipitisha
katika kila kiungo chake. Matiti, shingoni, mapajani na miguuni huku akimalizia
mgongoni kwa kulibenua nyuma na kulitembeza sehemu yote ya mgongo. Aliridhika.
Alilifuata kabati lake
na kutoa nguo. Kioo hakikuwa mbali. Alikifuata na kucheza nacho tena kama pacha
wake. Alicheka mwenyewe.
Alijiona amependeza.
Alitembea kwenda mbele na kurudi nyuma. Mwishowe alijiona mjinga. Alikimbilia
simu yake na kuzima taa tayari kufunga mlango na kuelekea kazini kwake.
USIKOSE SEHEMU YA PILI

No comments:
Post a Comment