SEHEMU YA PILI
Jane
alikuwa msichana anayejithamini sana. Hakujali watu wasemavyo juu yake wala
hakutaka kujisahau na kwenda kinyume na matarajio yake kwa siku nyingi.
Kujiamini ndiyo kitu alichokijua anacho. Hakuwaogopa wanaume wakware
waliomtamani na alilijua hilo. Utitiri wa wakware hao ulimfanya ajione
mlimbwende zaidi ya alivyosifiwa.
Kwa upande wa wanawake aliwajua pia. Hakuwajali wanawake waliokaa vibarazani na kumsema. Alijua alipotokea na alilolifanya. Ziada ingekuja baada ya kugundua jipya. Alilolipanga usiku asubuhi na kutwa nzima angelitekeleza. Hakuamini kama kuna kushindwa wala kukata tamaa. “Eti maisha magumu.”
“Mie aaah, kama hataki na aniache n'tarudi kwetu.... na ana ubavu huo? Mi kazi sifanyi na kila kitu analeta mwanamume wangu,” ni maneno ya dada mmoja tipwatipwa. Aliyeonekana kuupa nafasi msosi na maneno. Ambaye hakufanya lolote zaidi ya kukaa na kusubiri.
Siku hiyo Jane alibahatika kusikia maneno hayo. Aliyatafsiri na kusikitika.
“Mwanamke kukaa kumsubiri mwanamume alete! Mmh,” aliwaza huku akiwapita wanawake wale waliokuwa wamekaa nje ya nyumba zao.
Hayo maneno aliishia tu kuyasikia kwa watu lakini kwake hakuyaruhusu. “Mwanamke kupambana” ni maneno aliyosimama nayo na aliyoyaheshimu katika fikra zake na ndoto zake za kujiinua kimaisha.
Alikuwa wa namna ya pekee. Uzuri wake haukuwachosha wanaume wakware kumtazama. Machoni ukimtazama utatamani umweke ndani. Wanaume wengi walimtamani na hilo alilijua. Mvuto wake ni karibisho tosha kwa yeyote anayehisi maumivu ya moyo. Lakini utamwanzaje. Wengi wao walijiuliza bila ya kuwa na majibu kwani hakuna aliyekaribia kumpata Jane.
“Anatembea na wazungu na wanaume matajiri tu yule.”
“Hawa wakuja watamuweza?”
“Anajidai anaishi kizungu sana.”
“Inawezekana
ana ngoma hataki tujue. Mbona hata hashindi nyumbani.”
“Haeleweki, kila siku anafuatwa na magari ya
kifahari na kurudishwa. Ni Malaya yule dada, achene tu.”
“Na
ndo maana haeleweki, pengine mgonjwa na anasambaza kwa wakware wenye
kumtamani.”
“Ndo
maana hata na ukubwa wote huo haolewi.... yatamshinda.”
Hizo
ni kauli za wanawake kwa wanaume walivyomfikiria Jane.
*****
Ni
James tu ndiye aliyekuwa na mazoea na binti huyu,Jane. Alikuwa ni
mfanyabiashara. Mfanyabiashara aliyejituma na kuifanya kazi yake vizuri. Riziki
ya siku ilimtosha kuendesha maisha yake bila wasiwasi.
Alikuwa
na kibanda chake cha kukaanga chipsi maeneo ya Magomeni Mapipa ambacho
alikitegemea kusogeza siku. Watu wengi walikuwa wakifika hapo kupoza njaa zao.
Utaalamu wake wa kutengeneza chipsi ulimfanya awavute wateja wengi hata
kusababisha wengine wahamie kwake kutoka sehemu za awali walizokuwa wakinunua
chipsi. Hakutaka kuifanya kazi yake kuwa ngumu kwa kuwa mvivu. Ni kitu ambacho
hakupenda kukipa na fasi kimtawale. Hata wateja wake hawakuwa na wasiwasi juu
ya kupata huduma yake kwani aliwajali Zaidi.
Alimfahamu Jane kwa kuwa alikuwa mteja wake mkubwa sana. Ni nje ya nyumba aliyoishi Jane ndipo James alikuwa akiifanya biashara yake hiyo.
Alimfahamu Jane kwa kuwa alikuwa mteja wake mkubwa sana. Ni nje ya nyumba aliyoishi Jane ndipo James alikuwa akiifanya biashara yake hiyo.
Walitaniana
sana japo James hakufika kwa utani wa Jane. Jame alikuwa mwongeaji zaidi ya
James. Jane alitumia mwanya huo kukopa hata chipsi na kulipa baadaye. Kwa James
hilo halikuwa tatizo kwani Jane hakuwahi kumdhulumu kamwe. Alimwamini zaidi ya
wateja wake wote. Na siku zote lazima angeonana na Jane kabla au pindi arudipo
kutoka kazini kwake Kariakoo.
“Dada
Jane, habari za asubuhi,” James alimsalimia Jane.
“Nzuri
James umeamkaje,” Jane aliitikia salamu ya James huku akionekana mchovu sana.
Kwa nusu dakika James alikuwa amehisi baya kwa Jane. Hakuwa kawaida. Alionekana
kachoka sana hali iliyomfanya James, kumwangalia sana. Hakuwa yeye, ilibidi
aache alilokuwa akifanya na kumuuliza.
“Kulikoni
dada Jane leo nakuona tofauti, vipi mgonjwa au?” Jane hakuwa Jane aliyekuwa
akicheka mwenyewe na kioo chake. Aliyejibetua na kjishika kila mahali
akiufurahia uzuri wake. Hakuwa yeye tena. Alibadilika.
Ni
baada tu ya kutoka nje ndipo alipokumbuka yaliyomsibu. Hakutamani aione nje
hiyo kwani ndiyo huku huko alikupata masaibu hayo yaliyomfanya awe mnyonge.
“Acha
tu James,” Jane hakumwambia James juu ya kinachomsumbua. James hakutaka
kuendelea. Alijuwa huenda angemkera Jane, alibakia amesimama huku akimwangalia
Jane mbaye alikuwa akirudi ndani, aliendelea na kazi yake ya kukusanya masalia
ya mbao kwa ajili ya kuwashia moto ili aanze shughuli yake ya kupika chipsi.
Haikuwa
kawaida kwa wawili hao. Siku hiyo Jane aliondoka pasipo kumsemesha James. James
aliichukulia hali ile tofauti lakini aliapa lazima amuuulize hata kama ni kwa
kumlazimisha ajibu.
ITAENDELEA...


