HADITHI

Friday, July 31, 2015

HADITHI YA UTAMU WA ZEGE



SEHEMU YA PILI

Jane alikuwa msichana anayejithamini sana. Hakujali watu wasemavyo juu yake wala hakutaka kujisahau na kwenda kinyume na matarajio yake kwa siku nyingi. Kujiamini ndiyo kitu alichokijua anacho. Hakuwaogopa wanaume wakware waliomtamani na alilijua hilo. Utitiri wa wakware hao ulimfanya ajione mlimbwende zaidi ya alivyosifiwa.

Kwa upande wa wanawake aliwajua pia. Hakuwajali wanawake waliokaa vibarazani na kumsema. Alijua alipotokea na alilolifanya. Ziada ingekuja baada ya kugundua jipya. Alilolipanga usiku asubuhi na kutwa nzima angelitekeleza. Hakuamini kama kuna kushindwa wala kukata tamaa. “Eti maisha magumu.”

“Mie aaah, kama hataki na aniache n'tarudi kwetu.... na ana ubavu huo? Mi kazi sifanyi na kila kitu analeta mwanamume wangu,” ni maneno ya dada mmoja tipwatipwa. Aliyeonekana kuupa nafasi msosi na maneno. Ambaye hakufanya lolote zaidi ya kukaa na kusubiri.

Siku hiyo Jane alibahatika kusikia maneno hayo. Aliyatafsiri na kusikitika.
“Mwanamke kukaa kumsubiri mwanamume alete! Mmh,” aliwaza huku akiwapita wanawake wale waliokuwa wamekaa nje ya nyumba zao.

Hayo maneno aliishia tu kuyasikia kwa watu lakini kwake hakuyaruhusu. “Mwanamke kupambana” ni maneno aliyosimama nayo na aliyoyaheshimu katika fikra zake na ndoto zake za kujiinua kimaisha.

Alikuwa wa namna ya pekee. Uzuri wake haukuwachosha wanaume wakware kumtazama. Machoni ukimtazama utatamani umweke ndani. Wanaume wengi walimtamani na hilo alilijua. Mvuto wake ni karibisho tosha kwa yeyote anayehisi maumivu ya moyo. Lakini utamwanzaje. Wengi wao walijiuliza bila ya kuwa na majibu kwani hakuna aliyekaribia kumpata Jane.

“Anatembea na wazungu na wanaume matajiri tu yule.”
 “Hawa wakuja watamuweza?”
 “Anajidai anaishi kizungu sana.”
“Inawezekana ana ngoma hataki tujue. Mbona hata hashindi nyumbani.”
 “Haeleweki, kila siku anafuatwa na magari ya kifahari na kurudishwa. Ni Malaya yule dada, achene tu.”
“Na ndo maana haeleweki, pengine mgonjwa na anasambaza kwa wakware wenye kumtamani.”

“Ndo maana hata na ukubwa wote huo haolewi.... yatamshinda.”
Hizo ni kauli za wanawake kwa wanaume walivyomfikiria Jane.

*****
Ni James tu ndiye aliyekuwa na mazoea na binti huyu,Jane. Alikuwa ni mfanyabiashara. Mfanyabiashara aliyejituma na kuifanya kazi yake vizuri. Riziki ya siku ilimtosha kuendesha maisha yake bila wasiwasi.
Alikuwa na kibanda chake cha kukaanga chipsi maeneo ya Magomeni Mapipa ambacho alikitegemea kusogeza siku. Watu wengi walikuwa wakifika hapo kupoza njaa zao. Utaalamu wake wa kutengeneza chipsi ulimfanya awavute wateja wengi hata kusababisha wengine wahamie kwake kutoka sehemu za awali walizokuwa wakinunua chipsi. Hakutaka kuifanya kazi yake kuwa ngumu kwa kuwa mvivu. Ni kitu ambacho hakupenda kukipa na fasi kimtawale. Hata wateja wake hawakuwa na wasiwasi juu ya kupata huduma yake kwani aliwajali Zaidi.

Alimfahamu Jane kwa kuwa alikuwa mteja wake mkubwa sana. Ni nje ya nyumba aliyoishi Jane ndipo James alikuwa akiifanya biashara yake hiyo.
Walitaniana sana japo James hakufika kwa utani wa Jane. Jame alikuwa mwongeaji zaidi ya James. Jane alitumia mwanya huo kukopa hata chipsi na kulipa baadaye. Kwa James hilo halikuwa tatizo kwani Jane hakuwahi kumdhulumu kamwe. Alimwamini zaidi ya wateja wake wote. Na siku zote lazima angeonana na Jane kabla au pindi arudipo kutoka kazini kwake Kariakoo.
“Dada Jane, habari za asubuhi,” James alimsalimia Jane.
“Nzuri James umeamkaje,” Jane aliitikia salamu ya James huku akionekana mchovu sana. Kwa nusu dakika James alikuwa amehisi baya kwa Jane. Hakuwa kawaida. Alionekana kachoka sana hali iliyomfanya James, kumwangalia sana. Hakuwa yeye, ilibidi aache alilokuwa akifanya na kumuuliza.
“Kulikoni dada Jane leo nakuona tofauti, vipi mgonjwa au?” Jane hakuwa Jane aliyekuwa akicheka mwenyewe na kioo chake. Aliyejibetua na kjishika kila mahali akiufurahia uzuri wake. Hakuwa yeye tena. Alibadilika.
Ni baada tu ya kutoka nje ndipo alipokumbuka yaliyomsibu. Hakutamani aione nje hiyo kwani ndiyo huku huko alikupata masaibu hayo yaliyomfanya awe mnyonge.
“Acha tu James,” Jane hakumwambia James juu ya kinachomsumbua. James hakutaka kuendelea. Alijuwa huenda angemkera Jane, alibakia amesimama huku akimwangalia Jane mbaye alikuwa akirudi ndani, aliendelea na kazi yake ya kukusanya masalia ya mbao kwa ajili ya kuwashia moto ili aanze shughuli yake ya kupika chipsi. 
Haikuwa kawaida kwa wawili hao. Siku hiyo Jane aliondoka pasipo kumsemesha James. James aliichukulia hali ile tofauti lakini aliapa lazima amuuulize hata kama ni kwa kumlazimisha ajibu.


ITAENDELEA...

Wednesday, July 22, 2015

HADITHI YA UTAMU WA ZEGE

SEHEMU YA KWANZA



*****
MLIO wa simu yake ndiyo uliozindua kutoka katika ndoto yake ambayo hakuimalizia vizuri. Ndoto iliyoamsha tabasamu zuri kama aamkavyo kila siku akiwa na furaha. Furaha ya kupata kile akitakacho. Maisha aliyatamani na kuweza kuwa nayo.
Hakuwa na jinsi zaidi ya kutii amri ya simu yake. Alijiwekea alamu tayari kwa kumwamsha kila siku. Kaupepo kalichopenya dirishani pia hakikumpa nafasi ya kuendelea kujigubika na shuka. 
Alizitumia kama dakika tano kujiweka sawa kabla ya kutoka kitandani. Usingizi haukumweka tena kitandani. Alitabasamu tena kuushukuru upepo ulioumaliza usingizi wake na kumfanya mpya tayari kwa kuianza  siku hiyo. Alijivuta hadi kushika simu yake iliyokuwa katika kijimeza kidogo pembeni ya kitanda na kuiangalia. Hakukuta chochote zaidi ya nambari zilizoonyesha muda wa kuamka baada ya ile alamu kuisha.
Saa kumi na moja na nusu asubuhi ni muda ambao siku zote alijikuta yuko macho. Wakati mwingine aliiwahi alamu ya simu yake kabla haikulia kumwamsha. Hapo alijua labda ililia na hakuisikia na hivyo amechelewa. Alifurahi mara nyingi alipoiwahi. Alijua kulala sana ni dalili za uvivu na hivyo hakuupa nafasi uvivu umtawale.
Wakati mwingine hakuipenda kwani ingemaliza hamu yake ya kulala wakati bado ana usingizi, hivyo alijua siku za kuiweka na siku za kuitoa. Ni endapo angechelewa kulala sana. Asingeiweka na siku hiyo angeamka muda wowote na kwenda kazini.
Kama kawaida yake. Kioo kilikuwa ni kitu cha pili baada ya kuiwasha taa yake iliyokuwa karibu na kitanda. Taa inayowekwa mezani kwa ajili ya dharura. Mwanga hafifu uliomwangazia ulimtosha kujiangalia usoni peke yake. Alitaka kila siku aone mabadiliko yaliyotokea wakati akiwa amelala. Kama angeona utofauti, hakusita kwenda kwa mtaalamu ili amsaidie. Lakini leo hakuona lolote. Alijiona vilevile kama alivyolala jana yake saa tano na nusu usiku.
Kati ya mambo ambayo Jane aliyahusudu sana ni jinsi alivyo. Alijua ni hulka ya wanawake kujipenda lakini yeye aliona amewazidi kwa kujipenda alivyo. Kitu gani hakuwa nacho hadi asijihusudu mwenyewe pindi ajiangaliapo kwenye kioo chake mwenyewe...
Aliamka sasa na kukifuata kioo kikubwa alichokuwa amekiegemeza ukutani. Inawezekana kwa kuamka mapema kila siku ni ile autumie muda huo kucheza na kioo. Vyumba vyake viwili na maliwato iliyokuwa ndani ilimfanya ajisikie huru kama aishiye katika hekalu. Yote aliyafanya ndani. Alifurahia maisha yake. Alifanya alichokitaka.
Kioo chake hakukitumia vibaya. Sasa ilikuwa zamu ya umbo lake. Alikifuata kioo na kukisimamisha vizuri. Alijiona wote.  Alitoa shuka ambalo alikuwa amejifunika. Alilirusha hadi kitandani kama vile alisahau bahati mbaya akashuka nalo. Alisahau kwamba lilitakiwa limsitiri. Habari hiyo hakuitaka. Alisimama wima. Tabasamu lilianza kuchanua taratibu. Kila ajiangaliapo husahau kama alifanya hivyo jana yake. 
Alijitazama na kuliangaza umbo lake lililoimarika vizuri. Alijitamani. Alishika kiuno chake kwa staili ifanywayo na walimbwende wawapo katika mashindano. Kisha akatembea hatua mbili mbele. Alicheka. Alijikubali. Alitamani apige kelele kumshukuru aliyemleta duniani.
Alirudi tena hatua mbili nyuma. Sasa aligeuka kuangalia umbile lake kwa nyuma. Aliguna akimaanisha Muumba hakumkosea. Taratibu akawa anaelekea bafuni akiwa hajaridhika.
Alilifuata bafu huku macho yake yakiwa nyuma kumalizia kujitazama tena na tena kama hatatoka tena alikokwenda. Huko bafuni yakawa yale yale. Kila kiungo kikisafishwa kwa nafasi yake. Mikono yake laini ilipita kila sehemu kuhakikisha inapata sabuni iliyokuwa inanukia pamoja na maji.
Dakika kumi zilimtosha kujimwagia maji, si mkaaji sana wa bafuni. Alitoka. Alirudi tena kiooni. Sasa ilikuwa ni kujikausha kwa taulo lake jeupe na safi. Alifanya hivyo akilipitisha katika kila kiungo chake. Matiti, shingoni, mapajani na miguuni huku akimalizia mgongoni kwa kulibenua nyuma na kulitembeza sehemu yote ya mgongo. Aliridhika.
Alilifuata kabati lake na kutoa nguo. Kioo hakikuwa mbali. Alikifuata na kucheza nacho tena kama pacha wake. Alicheka mwenyewe.
Alijiona amependeza. Alitembea kwenda mbele na kurudi nyuma. Mwishowe alijiona mjinga. Alikimbilia simu yake na kuzima taa tayari kufunga mlango na kuelekea kazini kwake.
 USIKOSE SEHEMU YA PILI

Friday, July 17, 2015

KUHUSU SIMULIZI ZA KIAFRIKA

 TUNGO ZETU

Ni Simulizi za Kiafrika kwa Waafrika, blog inayokuletea Hadithi na machombezo tofauti kutoka kwa wataalamu wa Utunzi. Kwa watumiaji wa blog hii kama mdau unaweza kutuma hadithi yako na kuwekwa hapa kwa ajili ya kusomwa na wadau.
Pamoja na blog hii, pia kuna Ukurasa wa facebook wa TUNGO ZETU ambao unaendelea kutoa burudani kwa wadau wake.
Hapa tunakusogezea karibu namna ya kutupata kwa urahisi kama TUNGO ZETU ili uweze kupata ladha za hadithi mbalimbali na machombezo ya kusisimua kila siku.

Tuwe pamoja wadau. 

Mjulishe na mwenzako.























TUNGO ZETU